HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA PWANI TUMBI YAPATA MSAADA WA VIFAA TIBA
Posted on: January 20th, 2026
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani – Tumbi leo tarehe 21 Januari, 2026 imepokea vifaa vya kuokoa maisha ya watoto wachanga walioko katika hali hatarishi na wanaohitaji uangalizi maalum kutoka Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU). .
Akikabidhi mashine hiyo kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Tumbi Dkt Amaan K. Malima, Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Crispin Chalamila alisema, mashine hizo zimenunuliwa na wafanyakazi wa Takukuru kupitia michango wanayotoa kila mwaka kama sehemu ya kuwakumbuka watu wenye mahitaji maalum kama vile huduma za afya katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema,vifaa hivyo ni katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha huduma za afya kwa Watanzania na kuwataka wafanyakazi wa Hospitali hiyo kutunza vifaa hivyo ili viweze kusaidia katika kutoa huduma bora kwa watoto wachanga.
Alisema,Takukuru ipo tayari wakati wote kushirikiana na Hospitali ya Rufaa Tumbi ili kuona miradi inayotekelezwa katika Hospitali hiyo na nyingine hapa nchini inatekelezwa vizuri bila kuwepo vitendo vya ubadhilifu ili ikamilike kwa wakati na wananchi wapate huduma zinazostahiki.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali aliushuru uongozi na watumishi wa Takukuru kwa msaada waliotoa kwa hospitali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya ya mtoto na kwa kuwahidi vifaa hivyo vitatumika kwa uangalizi mkubwa na kwa manufaa kwa jamii.
Awali Daktari Bingwa wa watoto wa Hospitali ya rufaa Tumbi Dkt. Adelina Rutashobya alisema Hospitali ya rufaa Tumbi inatoa huduma kwa watoto ambao wamezaliwa kabla ya muda wa kuzaliwa ambao wanakabiriwa na changamoto mbalimbali ikiwemo manjano, maambukizi kwenye mfumo wa hewa na wenye uzito mdogo na changamoto nyingine mbalimbali.
Dkt. Rutashobya alieleza kuwa, huduma nyingine zinazotolewa ni kutunza Watoto wachanga ambao hawana changamoto za kiafya, lakini wazazi wao na wale ambao wamepoteza wazazi wanapata huduma mbalimbali.
“Watoto hawa wanapata huduma kama vile dawa, usaidizi wa kupumua, kwa njia ya tiba hewa (Oxygen) kutibu manjano kwa mashine maalum, kinga dhidi ya maambukizi ya magonjwa, kulishwa, kutunza joto la mwili kwa mashine na usafi wa mwili” alisema.
Vifaa hivyo, ambavyo ni phototherapy machine na infant radiant warmer, vitasaidia kuongeza uwezo wa hospitali katika utoaji wa huduma muhimu za dharura kwa watoto wachanga na kuboresha zaidi mazingira ya matibabu kwa watoto wanaohitaji uangalizi wa karibu


