Ukaribisho
Dr. Amaani K. Malima
Mganga Mfawidhi
Mabibi na Mabwana!
Ninayo furaha kubwa kuwakaribisha kwenye tovuti hii itakayowapa taarifa muhimu kuhusiana na Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Pwani-Tumbi .
Kabla ya yote kwa niaba ya familia ya Tumbi napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa utayari wako wa kutembelea tovuti hii na kujifunza kuhusu sisi. Nimatumaini yangu kuwa tovuti hii itakuwa msaada mkubwa kwa kuwapa taarifa muhimu kuhusu huduma zote za kitibabu zinatopatikana kwenye hospitali yetu na itatoa fursa ya kuwasiliana na wataalamu wa afya waliopo Tumbi.
Hospitali ilianzishwa mwaka 1967 kama zahanati iliyohudumia idadi ndogo ya watu na wafanyakazi wa mradi wa iliyokuwa Tanganyika-Nodik. Mnamo mwaka 1970 zahanati ilipandishwa kuwa kituo cha afya chenye uwezo wa kulaza wagonjwa 35. Kutokana na huduma nzuri zilizovutia jamii jirani ilipelekea mnamo mwaka 1996 kituo hiki kutunukiwa kuwa Hospitali Teule ya Tumbi. Baadae mwezi wanne 2011 Hospitali ya Tumbi ilipandishwa kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani na ilikuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa 230.
Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani Tumbi, ipo kilimeta 35 kutoka Mji wa Dar Es Salaam na kando ya barabara iendayo Morogoro na inahudumia takribani watu 1,162,431 kutoka wilaya tano za mkoa wa Pwani pamoja na Zahanati,Vituo vya Afya vilivyopo ndani ya Mkoa.
Hospitali yetu inajivunia kutoa huduma za kitibabu,mafunzo na tafiti. Huduma mbalimbali za kibingwa zitolewazo katika hospitali yetu ya Tumbi ni pamoja na Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Magonjwa ya Watoto, Sikio Pua na Koo, Upasuaji, mifupa, Magonjwa ya Ndani na huduma za Meno. Kwa mwaka Hospitali yetu inahudumia kiasi cha wagonjwa wa nje 144,000 na wagonjwa wa kulazwa 7200.
Pia tuna kliniki maalum kwa wanufaika wa mifuko ya Bima za Afya ambapo vipimo na matibabu yanapatikana .
Hospitali yetu inakada mbalimbali za wafanyakazi ambao wako tayari kukuhudumia wakiwemo Madaktari, Manesi, Wafamasia, Wataalamu wa Lishe, Wataalamu wa Maabara, wataalam wa huduma za Ustawi wa Jamii, Maafisa Afya, Utawala na Wahudumu wengine.
Ni matumaini yetu kuwa utembeleapo tovuti hii utapata taarifa muhimu kuhusu rasilimali watu, huduma za kitibabu zipatikanazo katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Pwani-Tumbi
Asante sana kwa kuchagua hospitali yetu.
Tunawatakia huduma njema
Dr. Amaan K. Malima
Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi