MAADHIMISHO YA MIAKA 58 YA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA PWANI TUMBI

Posted on: October 9th, 2025

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi imeadhimisha miaka 58 tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya shughuli mbalimbali zilizoanza tarehe 1 Oktoba, 2025 ambazo ni michezo iliyoanza kufanyika kuanzia tarehe 1 Oktoba 2025 kwa kuzishindanisha timu za karibu zinaozoizunguka Hospitali. Michezo hiyo ilikuwa ni  mpira wa miguu, mpira wa pete kwa wanawake, kuvuta kamba, kukimbiza kuku, na riadha. Aidha, michezo hiyo ilihusisha pia watumishi kutoka idara na vitengo mbalimbali ndani ya hospitali, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha umoja na mshikamano kazini.

Pamoja na shughuli hizo za michezo Hospitali pia iliandaa Kambi ya Huduma za Afya zilizotolewa bure kwa wananchi kwenye eneo la Mwendapole Wilaya ya Kibaha Pwani iliyoshirikisha watoa huduma za afya mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa kwenye maeneo yote muhimu kama vile Daktari bingwa wa Watoto, Daktari bingwa wa wanawake na Uzazi, Daktari bingwa wa Macho, Daktari bingwa wa Magonjwa ya Ajali na Dharura, Daktari bingwa wa Magonjwa ya ndani na Daktari bingwa masikio,pua na kinywa Pamoja na Huduma za uchangiaji damu. Sambamba na hilo kulikuwa na upimaji wa macho, shingo ya kizazi na Virusi vya Ukimwi. Kutokana na shughuli hizo zote walikuwepo pia Watalaamu wa Lishe,  washauri nasaha na wafamasia.

Kilele cha Maadhimisho hayo yalifanyika siku ya Jumamosi  tarehe 11 Oktoba 2025, ambapo yalianza na maandamano ya watumishi wa Hospitali ya Tumbi yaliyoshirikisha kila Idara na vitengo mbalimbali, ambapo zilitambulisha taaluma zao kwa mabango tofauti tofauti, pia yalibeba ujumbe muhimu  kuonesha majukumu yao mbalimbali yaliyopokelewa na mwakilishi wa Mgeni rasmi  Bi. Pili Mnyema, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani aliyokuja badala ya Mkuu wa Mkoa Mhe. Abubakar Kunenge.

Bi Pili kwa niaba ya  Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Aboubakar Kunenge, alitoa pongezi kwa uongozi wa hospitali kwa juhudi zao kubwa katika kuboresha huduma za afya na kuendelea kuwa nguzo muhimu katika  sekta ya afya. Na aliahidi kufanya kazi bega kwa bega na Hospitali ili kuwa hospitali bora ambayo itakayoweza kutoa huduma zote muhimu.

Aidha Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Kusirye Ukio alitoa pongezi kwa uongozi na watumishi wote wa Hospitali ya Tumbi kwa kuendelea kushirikiana na kuweka umoja mbele, nidhamu na kusisitiza kuwa ushirikiano huo ndio msingi wa mafanikio makubwa ya hospitali hiyo mpaka hivi sasa.

Kwa upande wake  Mganga Mfawidhi wa Hospitali  Daktari Amaani Malima, kwenye hotuba fupi iliyoelezea historia ya hospitali, changamoto zilizopo, mafanikio yaliyopatikana, na kutoa shukrani kwa viongozi na wadau wote waliounga mkono maendeleo ya hospitali hiyo. Dkt. Malima pia aliwashukuru watumishi wote kwa kujituma, kufanya kazi kwa bidii, na kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.

Kwenye kilele cha maadhimisho hayo kulifanyika hafla ya chakula cha jioni ilishoshirikisha watumishi kadhaa waliotoka kwenye utumishi wa umma ambao waliitumikia hospitali kwa kipindi hicho.