MAGEREZA MKOA WA PWANI WAADHIMISHA MIAKA 64 KWA KUTOA MSAADA HOSPITALI YA TUMBI
Posted on: August 25th, 2025
Tumbi Kibaha, Pwani Tarehe 25 Agosti 2025:
Katika kuadhimisha miaka 64 tangu kuanzishwa kwa Jeshi la Magereza Tanzania baada ya uhuru, wanajeshi wa Magereza kutoka Gereza la Mahabusu Mkuza, Kibaha Pwani wameendelea kuthibitisha dhamira ya kushirikiana na jamii katika kujenga afya na ustawi wa wananchi.
Leo hii wameonyesha dhamira yao kuu ambayo ni mshikamano na upendo, Jeshi la Magereza limeunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha afya za wananchi na kulinda mazingira.
Maafisa na askari wa Jeshi la Magereza walifika Hospitalini Tumbi na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii. Walianza kwa kusafisha mazingira ya hospitali, ikiwa ni sehemu ya kutunza afya na mazingira salama kwa wagonjwa na wananchi wote.
Akizungumza kwa Niaba ya hospitali Kaimu Mganga Mfawidhi, Dkt. Silas Msangi amewashukuru wanajeshi wa Magereza kwa mchango wao muhimu, ukielezwa kuwa ni kitendo kinachoonesha mshikamano, uzalendo na upendo kwa jamii.
Aidha, kama sehemu ya mchango wao kwa afya ya jamii, walitoa damu kwa hiari, wakitambua umuhimu wa damu salama katika kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji.
Kauli Mbiu ; “Ushirikiano wa Magereza na Jamii kwa urekebishaji wenye tija”.