TUMBI YAPOKEA VIFAA TIBA VYA MSAADA KUTOKA KOREA

Posted on: August 25th, 2025

Leo tarehe 25 Agosti, 2025 Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani – Tumbi imepokea vifaa tiba mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi 75,015,591.00 kutoka Taasisi ya Korea Foundation for international healthcare (KOFIH), msaada ambao utasaidia kuendelea kuimarisha na kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa wanaofika hospitalini hapa.

Vifaa tiba hivyo vitatumika kuendelea kuboresha huduma za dharura kwa wagonjwa, wagonjwa wanaofanyiwa upasuaji, kufuatilia mienendo ya wagonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji ili kuhakikisha afya zao zinaendelea kuimarika kwa wakati.

Akipokea msaada huo, Mganga Mfawidhi wa Hospitali Dkt. Amaan K. Malima ameshukuru kwa msaada huo kwani umekuja wakati muafaka na pia utaongeza ufanisi katika kutoa huduma na kuwafanya wananchi kuendelea kupata huduma bora.

Dkt. Malima ameongeza kuwa Taasisi kutoka Korea Kusini zimekuwa na ushirikiano wa manufaa makubwa na Muhimbili Mloganzila kwa kusaidia katika maeneo ya kuwajengea uwezo wataalam, kuleta wataalam kutoka Korea kwa lengo la kubadilishana uwezo pamoja na kutoa msaada wa vifaa tiba.

Kwa upande wake Mtalaamu wa Afya wa Taasis ya KOFIH Dkt.Hansol Park amesema taasisi yake wataendelea kutoa misaada kwa hospitali hii ili kuhakikisha Watanzania watapata huduma bora za afya.

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani – Tumbi imekuwa na ushirikiano wa muda mrefu na taasisi za Korea Kusini ikiwemo hii ya Korea Foundation for International Healthcare (KOFIH). Ambapo mara kadhaa wamekuwa wanatoa misaada vifaa tiba mbalimbali.