HUDUMA ZA SELIMUNDO ZAPATIKANA HOSPTALI YA TUMBI

Posted on: August 13th, 2025

Hospitali ya Tumbi imepongezwa kwa kutoa huduma sahihi kwa wagonjwa wa selimundu. Pongezi hizo zimetolewa leo tarehe 14 Agosti, 2025 na Dkt. Asteria V. Mpoto kutoka Wizara ya Afya Idara ya Magonjwa yasiyoambukizwa alipokutana na Wakuu wa Idara wa Hospitali ya Tumbi kwa lengo la kujadili na kupitia kwa pamoja mpango kazi wa Hospitali ili kuona upatikanaji wa vipimo, upatikanaji wa dawa pamoja na miundombinu sahihi kwa ajili ya kuwahudumia watu wenye tatizo la selimundu.
Katika msafara huo Dkt. Asteria aliambatana Madaktari watatu ambao ni Dkt. Adam Kilungu, Dkt. Jamila M. Makame na Godbles Mfuru ambao na wao pia ni wataalamu wa Afya katika eneo la ugonjwa wa selimundo. Akiongea kwenye kikao hicho Dkt. Asteria amesema kuwa Hospitali imeweka miundombinu sahihi katika utoaji wa huduma za wagonjwa wenye tatizo la selimundu.
Katika kikao hicho, DKt. Asteria ametoa ushauri kwa watendaji wa Hospitali kupata takwimu za wagonjwa wenye tatizo hilo ili kuwa takwimu sahihi za watu wanaokabiliwa na ugonjwa huo kwa kuweka mpango wa kuwapima Watoto wanaozaliwa Hospitalini hapa.
Kwa upanda wake Dkt. Pius Muzzazzi, Dakitari Bingwa wa Watoto na Kaimu Mganga Mfawidhi amewaeleza watalaamu hao kwamba Hospitali imekuwa ikiendesha kiliniki za Watoto wenye selimundu na ametumia nafasi hiyo kuwatangazia watu wote wa Jirani na hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi kuja kupima na kupata elimu ya uelewa juu ya ugonjwa wa selimundu.
Kabla ya kikao na Wakuu wa Idara watalaamu hawa wametoa mafunzo elekezi kwa watoa huduma wa upande wa Watoto wa Hospitali ya Tumbi, watoa huduma wa Maabara na watoa huduma wengine mbalimbali. Pia wamepata nafasi ya kutembelea sehemu mbalimbali za hospitali kama vile wadi za Watoto, Maabara na Maduka yanayotoa huduma za dawa.